WAZIRI JAFO AKUTANA NA WADAU WA MAZINGIRA KUTATUA KERO ZA MCHAKATO WA TATHMINI YA ATHARI KWA MAZINGIRA (TAM/EIA)


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Selemani Jafo, amekutana na wadau wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira ikiwa ni pamoja nawawekezaji, washauri elekezi wa Mazingira pamoja na wawakilishi wa Serikali kutoka Wizara mbalimbali zinazohusika katika mchakato wa kutoa cheti cha Mazingira. Mkutano huo Umefanyika ukumbi wa Kisenga, Millenium Tower, Kijitonyama Jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo umehudhuriwa na Waziri wa Uwekezaji Mhe. Geofrey Mwambe,Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu kazi na Vijana Mhe. Protabas Katambi, Naibu Waziri Wizara ya Viwanda na Biashara Mhe. Silaoneka Kigali Naibu katibu Mkuu Mohammed Abdallah Khamis,Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt.Andre Komba, Mwenyekiti wa Bodi ya NEMC Prof. Muhandisi Esnat Chaggu na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Muhandisi Samuel Gwamaka pamoja na wafanyakazi wa NEMC.

Mhe. Jafo akiwa Mwenyekiti katika mkutano huo ameeleza kuwa madhumuni makubwa ya mkutano ni kujaribu kuwekana sawa baina ya wawekezaji, washauri elekezi pamoja na watendaji wa Wizara yake ili kuepusha malalamiko na changamoto zinazojitokeza kipindi cha kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA).

Ameendelea kusema kuwa kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM/EIA) ni takwa la Kisheria na amebaini watu wengi hawajui umuhimu wa kufanya TAM/EIA, hivyo ameomba kila mtu kuwa balozi wa kutoa elimu hiyo.

"Nashukuru hapa watu wengi wanasema suala la uelewa kuhusu umuhimu wa TAM/EIA lipo chini ni kweli lipo chini na hivyo kupelekea watu wengi kufoji cheti cha mazingira na mwisho wa siku akija kutekeleza mradi wake anakuwa na changamoto nyingi za kimazingira na uwekezaji huo kuweza kuwa na hasara kwa mwekezaji na katika taifa letu kutokana na kutokufata utaratibu, hivyo naomba kila mtu akatoe elimu ya umuhimu wa mchakato huu kwa manufaa ya Taifa hili na kwa uzalendo" Amesema Mhe. Jafo.

Ameendelea kusema kuwa Serikali za Mitaa ziwe makini katika kutoa maeneo ya uwekezaji kwa kuwapa wawekezaji maeneo ambayo hayataleta migogoro na amewataka wawekezaji kuwekeza katika maeneo yalio rafiki kwa uwekezaji kuepusha migogoro katika jamii.

"Nawaomba Serikali za Mitaa kutenga maeneo ambayo hayana changamoto kubwa katika uwekezaji, NEMC na Ofisi yangu ya Makamu wa Rais hatutaruhusu uwekezaji ufanyike katika maeneo ambayo yataathiri mazingira na kuhatarisha maisha ya watu. Tunahitaji uwekezaji wa kila aina lakini kipaumbele cha mazingira kiwe cha kwanza katika uwekezaji wetu" Amesema Mhe. Jafo

Kwa upande wake Waziri wa Uwekezaji Mhe. Geofrey Mwambe amesemamfumo wa utoaji wa vibali uangaliwe vizuri ili kuwe na kituo kimoja ambacho kitakuwa na Wizara zote za Kiserikali ili muwekezaji aweze kupata vibali vyote hapo ili kuepusha mlolongo mrefu kwa muwekezaji hii itapunguza ukiritimba uliopo na kuondoa usumbufu kwa wawekezaji na kupelekea kuongeza uwekezaji Nchini na kukuza pato la Taifa.

Naye Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Ajira na Vijana Mh. Protabas Katambi, amesema kuwa katika andiko lililowasilishwa amebaini kuwa kwa hali ya kawaida tunaweka kipaumbele suala la uwekezaji bila kutazama mazingira yanayotuzunguka hivyo matokeo yake kusababisha madhara makubwa katika jamii.

Kwa upande wake Naibu Waziri Wizara ya Viwanda na ajira Mhe. Silaoneka Kigali amesema kuwa anaahidi kutoa ushirikiano wa dhati katika muktadha wa kujenga uchumi wa viwanda kwa kuhakikisha wanasimamia uchumi wa viwanda wenye mazingira bora na endelevu. Ameendelea kusema kuwa changamoto za kimazingira katika viwanda ni kubwa ndio maana kunahaja ya kuweka mikutano kama hii kuona namna gani tunapunguza athari kutokana na uwekezaji katika viwanda.

Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Prof. Muhandisi Esnat Chaggu amesema kuwa tunahitaji uwekezaji lakini uwekezaji wenye tija kwa Taifa letu, hivyo kila mmoja ni mdau wa utunzaji wa mazingira kwa manufaa ya Taifa

"Mazingira ni suala la muhimu kwa faida ya kizazi kilichopo na kijacho hivyo kila mtu ni mdau wa mazingira haya"Prof. Esnat

Naye Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Muhandisi Samuel Gwamaka amesema kuwa mchakato wa kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM/EIA) sio wa mshauri elekezi tu bali ni ushirikiano kati ya muwekezaji na Mshauri wake pamoja na NEMC.

"Wawekezaji wengi wanapotaka kupata cheti cha mazingira hawajihusishi sana katika utekelezaji wa mchakato huo hivyo kuwaachia kila kitu washauri elekezi na matokeo yake Muwekezaji kutofahamu anatakiwa kutekeleza yapi na hatimaye kutoa ushirikiano mdogo kwa mshauri wake" Dkt. Gwamaka

Ameendelea kusema kuwa muwekezaji anatakiwa kufahamu wajibu wake katika mchakato wa TAM/EIA ikiwemo kusimamia mchakato mzima. Pia ahakikishe ana umiliki halali wa ardhi na uwekezaji wake ulingane na matumizi ya ardhi pamoja na kuwa na mahusiano mazuri na majirani zake katika eneo analotakakuwekeza.