WANAFUNZI WA CHUO CHA TEKNOLOJIA CHA DAR ES SALAAM (D.I.T) WATEMBELEA NEMC KUJIFUNZA KUHUSU TATHMINI YA ATHARI KWA MAZINGIRA.


Wanafunzi wa Chuo cha Teknolojia cha Dar es Salaam, (DAR ES SALAAM INSTITUTE OF TECHNOLOGY) D.I.T wametembelea Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kujifunza namna ambavyo Baraza linaendesha shughuli zake katika upande wa TATHMINI YA ATHARI KWA MAZINGIRA. Wanafunzi hao waliambatana na Dkt. Mwanaisha Mkangara kutoka Taasisi ya Teknolojia DIT na kupokelewa na Mkurugenzi wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira NEMC Makao Makuu Dkt. Menan Jangu.

Akiongea baada ya kikao cha kutoaElimu kuhusu Tathmini ya Athari kwa Mazingira Dkt. Menan ametoa pongezi kwa Uongozi wa Chuo cha Teknolojia cha Dar es Salaam (DIT) kuwapa fursa wanafunzi kutembelea Ofisi za Baraza ili kupata ujuzi kuhusu umuhimu wa kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira jambo ambalo litawasaidia kuwa mabalozi wa maswala ya Mazingira katika jamii wanazoishi, jambo ambalo litasaidia kupunguza au kumaliza kero zinazo sababishwa na uharibifu wa mazingira.

“Naupongeza sana Uongozi wa DIT kwa kuliona hili suala kuwa ni la muhimu kwa kuwaruhusu hawa vijana kuja NEMC kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu taratibu za kisheria zinapaswa kuzingatiwa kabla ya kuanzisha miradi ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza na kuathiri hasa katikaAfya na Mazingira yetu, aidha uchumi endelevu unategemea pia mifumo thabiti ya Usimamizi wa mazingira.”

Dkt. Menan ameongeza kuwa vijana wana mchango mkubwa kwa jamii zinazowazunguka hivyo kuja kwao NEMC kwa ajili ya kupata ujuzi kuhusu Usiamizi na Uhifadhi wa Mazingira kwa ujumla ni habari njema kwasababu elimu hii itawafikia wengine kupitia vijana hao.

“Vijana ndiyo nguvu kazi ya Taifa na pia ndio tunawategemea kuwa mabalozi wazuri kwa jamii kuifikisha elimu hii waliyoipata, sambamba na hilo nina imani ujuzi huu utafanyika kwa vitendo na itapunguza athari zinazojitokeza katika mazingira yetu.”

Dkt. Menan ametoa wito kwa kwa vijana katika ngazi zote za elimu kushirikiana na Baraza katika kupata elimu kuhusu mazingira kama walivyofanya D.I.T. na kuisambaza.

“Natoa wito kwa wadau wote Elimu pamoja na Taasisi kushirikiana na NEMC katika kutatua changamoto mbalimbali za mazingira kupitia kupashana habari au kuelimishana ili kupunguza uharibifu wa mazingira. Nawakaribisha sana NEMC hii ni Taasisi ya Serikali hivyo ni yetu sote.”

Nae Dkt. Mwanaisha Mkangara kutoka Chuo cha Teknolojia cha Dar es Salaam DIT, amesema lengo la kuja NEMC ni kuja kupata ujuzi kuhusu somo la Tathmini ya Athari kwa Mazingira kwa wanafunzi wa stashahada mwaka wa pili, kwahiyo kabla ya kuwapima kwenye mitihani waliamua kuwaleta NEMC ili kufahamu kwa upana mambo yote yanayohusu Tathmini ya Athari kwa Mazingira sababu wanafunzi hao ndiyo watalaamu wa baadaye wa mambo yanayohusu mazingira, amesema Dkt. Mkangara.

“Tumewaleta Wanafunzi hapa NEMC lengo ni kuwajengea uwezo na ufahamu zaidi kuhusu Tathmini ya Athari kwa mazingira, hii ni fursa kwa wanafunzi kujifunza mambo ya mazingira kwasababu wao ndiyo wataalam, watumishi na viongozi wa baadaye kwenye Taifa letu hivyo ni jambo zuri kupata mafunzo haya kutoka NEMC.