WAITARA AVITAKA VIWANDA VYOTE NCHINI KUFANYA UKAGUZI BINAFSI WA KIMAZINGIRA KILA MWAKA.


Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Mwita Waitara, amesema kuwa kuna haja ya viwanda vyote vilivyopo Nchini kujiwekea utaratibu wa kufanya ukaguzi binafsi katika viwanda vyao ili kuepusha uchafuzi wa mazingira. Ameyasema hayo alipokuwa katika ziara ya ukaguzi wa mazingira katika kiwanda cha Fujian kinachozalisha Nondo kilichopo Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani. Amesema kuwa ni vizuri kufanya ukaguzi binafsi wa kila mwaka ili kuona namna gani kiwanda kinafanya kazi bila ya uchafuzi katika mazingira yetu.

Waitara amesema kuwa viwanda vingi vinapopata cheti cha mazingira havitekelezi masharti waliyopewa na NEMC na hii inapelekea kusababisha migogoro ndani ya jamii. Hivyo ni vizuri kufanya ukaguzi wa kila mwaka ili kuepusha malalamiko yanayotolewa na Wananchi.

"Suala la kimazingira ni suala la kila mtu na sio la mtu binafsi au Taasisi Fulani, kwani tusipohakikisha tunasimamia mazingira yetu ipasavyo miaka ya mbeleni tutakuwa hatarini" amesema Waitara.

Ameendelea kusema kuwa kiwanda cha Fujian ni kiwanda ambacho kinalalamikiwa na Wananchi wanaokaa karibu na kiwanda hicho kwa miaka mingi na kupelekea migogoro baina ya mwekezaji na jamii inayomzunguka, hii ni kutokana na wamiliki wa kiwanda kutojiwekea utaratibu wa kujikagua kila mwaka na kutofuata masharti waliyopewa na NEMC baada ya kupewa cheti. Changamoto nyingine ni kutokuwa na mtaalamu wa mazingira ambaye ataweza kumshauri mwekezaji namna ya kulinda mazingira.

"NEMC wamekuja hapa mara kadhaa na hata Mawaziri waliopita wamekuja hapa sana na kuna maelekezo yametolewa japo kuna baadhi yamefanyika lakini mengine bado hayajafanyika, hivyo namuagiza Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga na watendaji wake kuhakikisha kiwanda hikikinatekeleza maelekezo yote waliyopewa. Pia namuagiza Mkurugenzi Mkuu wa NEMC kusimamia na kuhakikisha kila kiwanda Nchini kinakuwa na Mtaalamu wa mazingira ili kuepusha changamoto za kimazingira na migogoro na jamii" amesema Waitara.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Mhe. Filberto Sanga amesema kuwa ni kweli malalamiko ya Wananchi juu ya kiwanda hiki ni ya muda mrefu lakini mwekezaji yuko tayari kulipa fidia kwa baadhi ya watu walio karibu na kiwanda hicho ili kuepusha malalamiko na athari kwa wakazi hao.

"Ombi langu kwa Watanzania kabla ya kujenga wanatakiwa kujiridhisha kuwa eneo analotaka kujenga ni katika maeneoyaliotengwa kwa ajili ya viwanda na sio makazi ili kuepusha malalamiko kama yanayojitokeza katika kiwanda hiko cha Fujian. Lakini pia naomba Taasisi pamoja na Wizara husika tushirikiane ili tuweze kuhakikisha makazi ya watu hayajengwi kwenye maeneo ya viwanda na maeneo yenye watu wengi kusiende kujengwa viwanda. Kama tutafanya hivyo matatizo haya hayatajitokeza tena." Amesema Filberto.

Kwa upande wake Meneja wa Mashariki Kusini (NEMC) Taimur Kisiwa, amesema kuwa kiwanda cha Fujian kilishakaguliwa kipindi cha nyuma na kubaini changamoto kubwa iliyopo ni malalamiko ya wananchi juu yamoshi unaotoka katika kiwanda hicho na kwenda kwenye makazi ya watu. “Kutokana na malalamiko hayo tulizungumza na mmiliki na kumtaka azuie moshi huo kwa kuweka mitambo ya kisasa ambayo itazuia moshi kwenda kwenyemakazi ya watu, pia watoe fidia kwa wakazi hao waweza kuhama ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima.

Vile vile Mhe. Waitara ametoa angalizo kwa Watanzania kuwa kugushi cheti cha Mazingira ni kosa kisheria endapo mtu atabainika anafanya hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa. Hivyo kila Mwekezaji ahakikishe anapata cheti ambacho ni halali na sio cha kughushi.

Mhe.Waitara amekamilisha ziara yake leo katika Mkoa wa Pwani, lakini amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Mhe.Filberto Sanga, pamoja na Mkuu wa kikosi cha ulinzi na usalama cha Mkurangakuhakikisha kiwanda cha Bubujao kilichopo Wilaya hiyo kinachukuliwa hatua kwa kugushi Cheti cha Mazingira.