UTIRIRISHAJI WA MAJI TAKA KWENYE MAZINGIRA NI KOSA KISHERIA- WAITARA


Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhe.Mwita Waitara, amesema kuwa utiririshaji wa maji taka toka viwandani na kupeleka kwenye mazingira bila ya kuyatibu ni kosa kisheria. Ameyasema hayo alipokuwa katika ziara ya ukaguzi wa mazingira katika kiwanda cha Keds Tanzania Company Limited kilichopo Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani.

Aidha Mhe. Waitara amesema kuwa kuna malalamiko mengi sana kutoka kwa Wananchi wanaokaa karibu na kiwanda cha Keds ambacho kinatiririsha maji machafu katika mfereji uliopo karibu na makazi yao. Ameeleza kuwa katika ziara yake amebaini utiririshaji wa maji machafu yanayotokana na maji ya mvua yanayoingia katika makaa ya mawe na kuingia kwenye mfereji uliopo ndani ya kiwanda na kwenda kwenye makazi ya watu

"Tumepokea malalamiko mengi kutoka kwa Wananchi hasa wanaoishi karibu na kiwanda hiki, kuna mfereji wa maji hapa, wakati wa mvua haya makaa ya mawe yanayotumika hapa yanachanganyika na maji ya mvua alafu yanaingia kwenye makazi yao. Sasa nimekuja hapa kwenye kiwanda na kweli nimebaini kuna maji ambayo yamechanyanyika na maji ya makaa ya mawe na kusababisha kuingia kwenye mazingira.” Alisema Waitara

Mhe. Waitara ametoa siku kumi na nne (14) kwa kiwanda hicho kuyafanyia kazi maagizo waliyopewa na NEMC na kuhakikisha wanaacha mara moja kutiririsha maji machafu kwenye mazingira kwani wanahatarisha usalama wa wananchi kiafya pamoja na kuharibu mazingira yetu. Pia Mh. Waitara amekitaka kiwanda hicho kuwa na mtambo wa kuchakata taka ambazo wanazalisha ili kuepusha kusambaa hovyi kwa taka.

“Kwa kuwa hiki kiwanda ni kikubwa ni muhimu sana kuwa na mtambo wa kuchakata taka ambazo zinazaliswha hapa haswa zisizo oza. Hivyo mkiwa na mtambo wenu itasaidia sana kutozagaa kwa taka hizi katika mazingira yetu, lakini pia mkiwa na mtambo huo hakikisha moshi hauzagai na kupelekea kuwa kero kwa wakazi wa eneo hili”Alisema Waitara.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Utekelezaji na Uzingatiaji wa Sheria (NEMC) Edger Mgila, amesema kuwa kiwanda cha Keds kinatumia makaa ya mawe kama chanzo cha nishati jambo ambalo ni zuri katika njia ya utunzaji wa mazingira, lakini shida iliyopo katika kiwanda hiki ni namna ya kuhifadhi makaa hayo.

“Kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wakazi wa maeneo ya jirani juu ya maji machafu kutoka kiwandani kuharibu mazingira. Tulichukua hatua ya kumuelekeza Mwekezaji namna ya kuhifadhi makaa hayo na tulitoa muda wa kuhakikisha hawatiririshi maji kwenda kwenye mazingira. Sambamba na hayo tulimkataza kuchoma taka katika eneo la wazi kwa kuwa moshi wake unaathari katika mazingira na afya za watu.” Alisema Edgar.

Vile vile Mhe. Waitara ametembelea kiwanda cha Sunda Chemical fibres, Fixing paper Manufacturing (T) Company Ltd, Kiluwa Steels Group Company Limited na kubaini kuwa viwanda hivyo vina vyeti vya mazingira lakini utunzaji wa mazingira haupo sawa hasa kwa upande wa maji taka. Ameiagiza NEMC kufanya ukaguzi katika viwanda vyote vilivyopo Kibaha Mkoa wa Pwani ili kuona kama taratibu na muongozo waliopewa baada ya kupewa cheti kama unazingatiwa.

“Natoa wito kwa NEMC wafanye ukaguzi wa viwanda vyote vya Wilaya hii ya Kibaha kwa kuwa inaonekana kuna mambo hayapo sawa, kuwapa cheti sio tatizo lakini ni lazima kufanya utekelezaji wa utunzaji wa mazingira kwa kuzingatia cheti walichopewa. Tunapenda wawekezaji lakini pia sheria ya Nchi lazima ifuatwe.” Amesema Mh. Waitara.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kilangalanga Mhe. Mwajuma Denge, amesema anamshukuru Mhe. Naibu Waziri kufanya ziara katika eneo hilo, kwani viwanda hivyo vimekuwa kero sana katika utunzaji wa mazingira lakini pia viwango wanavyolipwa wafanyakazi ni vidogo sana na havilingani na kazi wanazofanya na ikitokea mfanyakazi anaumia inakuwa shida katika kupewa matibabu.

“Kutokana na ujio wako na mimi nimepata nafasi hii ya kutoa kilio changu cha siku nyingi juu ya vijana wetu wanaofanya kazi katika viwanda hivii. Wanawatumikisha sana lakini katika ulipwaji umekuwa shida kwani wanalipwa fedha kidogo ambazo hazilingani na kazi wanazofanya. Ombi langu waangalie namna ya ulipwaji kama kuna muongozo wa kiserikali basi walipwe kulingana na muongozo huo ili kuepusha unyonyaji.”

Naibu Waziri Mhe. Waitara yupo katika ziara ya siku mbili katika Mkoa wa Pwani kujionea hali ya kimazingira katika mkoa huo