NEMC YATOA UFAFANUZI KUHUSU KATAZO LA VIFUNGASHIO VISIVYOKIDHI VIWANGO


Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC kwa kushirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wamekutana na wadau mbalimbali wa mazingira wakiwemo, wenye viwanda, wafanyabiashara na Shirikisho la Viwanda nchini, ili kutoa ufafanuzi kuhusu katazo la vifungashio vya plastiki lililotolewa na Baraza hilo hivi karibuni.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Mikocheni jijini Dar Es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Mhandisi Dkt. Samuel Gwamaka Mafwenga amesema Baraza limekutana na wadau wa mazingira, watengenezaji, wasambazaji nawatumiaji wa vifungashio baada ya kuona kwamba sasa hivi kumekuwa na ongezeko la vifungashiovya plastiki visivyokidhi viwango. Hii ni kinyume cha Sheria ya Mazingira na Kanuniza Katazo la mifuko ya plastiki ya mwaka 2019, ambazo Baraza ina jukumu la kuzisimamia.Katika mkutano huo NEMC naTBS wametoa elimu na kufafanua kwa wadau aina ya vifungashio vilivyokatazwa kuwa ni vile ambavyo havijakidhi viwango kwa mujibu wa sheria wala kuthibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania TBS. Sambamba na hili lengo lingine la mkutano huo lilikuwa ni kujadiliana njia bora ya kutekeleza katazo hili bila kuleta atharikubwa kiuchumi wala kuvunja Sheria.

“ Tamko letu liliwataka wenye viwanda kuzalisha vifungashio ambavyo vinakidhi viwango, vinarejelezeka pamoja na kuwa na lebo iwe rahisi kumtambua mzalishaji ili kudhibiti usambaaji wa vifungashio hivyo katika mazingira yetu. Vifungashio vingi vinavyozalishwa havina lebo ya mzalishaji wala bidhaa inayokusudiwa kufungashiwa na pia haviwezi kurejelezeka, jambo ambalo ni kinyume cha Sheria na hali hii inayafanya mazingira yetu kuchafuliwa na pia linaondoa usawa wa kibiashara kwa wale ambao wamekuwa wakizalisha vifungashio mbadala ambavyo ni rafiki kwa mazingira”. Dkt. Gwamaka alisema.

Nae Mkurugenzi wa Upimaji na Ugezi kutoka TBS Mhandisi Johannes Maganga amesema TBS itahakikisha inasimamia ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchini kwa mujibu wa Sheria kwa kushirikiana na Taasisi za Serikali kama NEMCna wadau wengine wote. "Zaidi ya kusimamia Sheria, TBS pia inatoa ushauri kwa wazalishaji pale ambapo kunakuwa na mapungufu yanayotokana na uzalishaji wa bidhaa, hivyo tutafanya kazi kwa karibu na wadau wote hususan wenye viwanda vya vifungashio na kuwapa vibali pindi watapokidhi vigezo vilivyowekwa kisheria". Alisema Mha. Maganga.

Fransisca Joseph Lyimo ambae ni mfanyabiashara wa vifungashio ameiomba Serikali inapokuwa inatunga Sheria iwashirikishe wadau ili kuepuka uvunjwaji wa Sheria usio wa lazima. Lengo ni kujenga nchi ya viwanda hivyo amemshukuru Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Gwamaka kwa kutoa ufafanuzi juu ya sheria na kanuni za vifungashio vinavyotakiwa kuzalishwa na kusambazwa pasipo kuleta madhara kwa mazingira na kwa wafanyabiashara.

“Vifungashio ni muhimu kwenye uchumi wa Viwanda lakini pia Sheria inapaswa ifuatwe na mazingira yatunzwe kwa manufaa yetu na vizazi vijavyo".Alisema Lyimo.

Abdallah Mwinyi, Katibu Mkuu Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania amesema wao wanaosimamia wajasiriamali wadogo na wa kati wanapaswa washirikishwe kwenye utungwaji wa sheria na kanuni kama hizi ili zinapokuja kutumika ziwe na sehemu ya mapendekezo yao, hii itasaidia sheria kutekelezeka kwa urahisi.