MKURUGENZI MKUU WA NEMC AWAALIKA WADAU WOTE KATIKA MKUTANO WA MASUALA YA EIA JIJINI DAR ES SALAAM


Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Dkt. Muhandisi Samuel Gwamaka, amewaalika wadau wote ikiwemo wawekezaji, washauri elekezi wa Mazingira na Taasisi binafsi katika mkutano wa kujadili masuala ya ucheleweshwaji wa mchakato wa kufanya tathmini ya athari kwa mazingira (EIA), mkutano huo utafanyika siku ya jumamosi 17/4/2021 saa tatu asubuhi katika ukumbi wa Kisenga Millenium Tower Kijitonyama, jijini Dar es Salaam

Akiongea na Waandishi wa Habari ofisi za NEMC Mikocheni jijini Dar es Salaam, Dkt. Gwamaka amesema kuwa ameitisha mkutano huo ikiwa ni maelekezo ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani Jafo, kutaka kukutana na wadau hao ili kutambua changamoto gani zipo katika mchakato wa kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA)

“Kama tunavyotambua kuwa mchakato wa kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira ni wa Kisheria kwa Miradi yote ya maendeleo ambayo haijajengwa inatakiwa kupitia mchakato huo ili upate cheti cha mazingira ambacho kinatolewa na Waziri mwenye dhamana ya mazingira. Kupitia mchakato huu kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wadau hivyo mkutano huu unaohusisha walengwa utasaidia kupata maoni ili kuweza kurekebishwa na mchakato huo kuwa mwepesi kwa maendeleo ya Taifa letu” amesema Dkt Gwamaka

Aidha Dkt. Gwamaka amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita haina malengo ya kukwamisha maendeleo katika Taifa hivyo mkutano huu umeitishwa kwa lengo la kutathmini ni wapi panahitaji kurekebishwa ili uwekezaji usikwamishwe kwa sababu zisizo za msingi.

“Naomba nitoe wito niwakaribishe wadau wote wanaohusika na mazingira siku ya Jumamosi tarehe 17 ukumbi wa kisenga Millenium Tower, jijini Dar es Salaam ili tuweze kukutana na kuweza kufanya mkutano wa pamoja hatimaye tuweze kuboresha utendaji mzima wa Serikali katika maeneo yote yanayohusiana na EIA”.

Katika hatua nyingine Dkt. Gwamaka amesema suala la vifungashio vya plastiki visivyo na viwango kwa sasa limefikia mwisho na endapo mtu akikutwa anauza au kutumia vifungashio vya plastiki ambavyo havijakidhi viwango hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

“Hatutegemei kuona kifungashio kisichokua na kiwango, elimu imeshatolewa vya kutosha na tulifanya kikao na Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) na wametuhakikishia kwamba viwanda vipo na vinatengeneza vifungashio vyenye kiwango kulingana na matumizi ya mtumiaji. Hivyo ukikutwa na kifungashio hakijakidhi kiwango utachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria. Kanda zote za NEMC Tanzania wameshaanza ukaguzi na utekelezaji unafuata endapo tutabaini mtu anauza au kutumia vifungashio visivyo na viwango” alisema Dkt Gwamaka

Ameendelea kusema kuwa ni vizuri kutekeleza sheria pasipo shuruti kwani elimu imeshatolewa vya kutosha endapo ukichukuliwa hatua usilaumu. Dkt Gwamaka amesema vifungashio hivyo visigeuke kuwa vibebeo na endapo utakutwa na kifungashio ambacho kimekidhi vigezo lakini umegeuza kibebeo hatua kali zitachukuliwa.