MARUFUKU KUZALISHA KARATASI ZA PLASTIKI KWENYE MFUNIKO WA CHUPA ZA MAJI-Mhe. JAFO


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani Jafo, amepiga marufuku uzalishaji wa karatasi ya plastiki kwenye Mfuniko wa chupa za maji na vinywaji vingine kwani vinachangia ongezeko kubwa la uchafuzi wa Mazingira katika Nchi yetu.

Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari katika ofisi za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) zilizopo Mikocheni jijini Dar es Salaam leo hii. Amesema kumekuwa na uzalishaji wa vifungashio laini vya plastiki kwenye vifuniko vya maji ambavyo haviwezi kurejerezeka na kusababisha kusambaa hovyo kwenye mazingira yetu.

Aidha ameeleza kuwa Serikali inaendelea kusitisha baadhi ya matumizi ya bidhaa za plastiki ambazo zinaendelea kutumika Nchini bila ya kurejelezeka. Mhe. Jafo amesema kuwa vikaratasi hivyo vinavyowekwa kwenye kifuniko cha chupa bado vinaathari kubwa katika mazingira hasa katika maeneo ya mazalia ya Samaki ambapo Samaki hao wanakula vikaratasi hivyo pamoja na wanyama ambavyo Ni hatari kwa maisha yao. Vilevile vikaratasi hivyo vinazagaa hovyo katika mifereji pamoja na kwenye fukwe kitendo ambacho ni hatari sana kwa viumbe na uhifadhi wa mazingira kwa ujumla.

“Hivyo kwa Mujibu wa Sheria yetu Serikali imepiga marufuku plastiki laini katika vifuniko vya chupa za vinywaji vyote vinavyozalishwa Nchini na zinazoingizwa Nchini, hivyo baada ya miezi sita kuanzia tarehe 11 Oktoba 2021 hatutegemei kuona karatasi hizo zinawekwa kwenye chupa ya kinywaji chochote.” amesema Mhe. Jafo

Ameendelea kusema kuwa marufuku kuzalisha au kuingiza mirija ya aina ya plastiki hivyo, tunatakiwa kutumia mirija mbadala ambayo inarejerezeka. Mirija mingi inayotumika hivi sasa ndani ya Nchi yetu hairejerezeki na inasababisha uchafuzi mkubwa wa mazingira hivyo amewataka wafanyabiashara na wajasiriamali kutumia mirija ambayo inarejerezeka ili kulinda mazingira yetu.

“Kutokana na changamato hizo tunatoa maelekezo kwamba wenye hoteli, Migahawa, baa, maduka mbalimbali yanayouza vinywaji kutotumia mirija ya plastiki ambayo hairejerezeki. Tumetoa muda wa miezi sita kuacha matumizi ya mirija ya plastiki isiyorejerezeka hivyo namuelekeza Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC wasimamie utekelezaji wa maagizo haya kama utaratibu unavyoelekeza” Amesema Mhe. Jafo