KILA MWANANCHI AENDELEE KULINDA MAZINGIRA KWA MUSTAKABALI WA NCHI YETU-Mhe.JAFO


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani Jafo, amesema kila Mwananchi ashiriki katika kulinda na kuhifadhi mazingira kwa mustakabali wa Nchi ili iendelee kubaki salama. Suala la Mazingira ni jambo kubwa sana linahitaji ushiriki wa kila mtu katika kusimamia na kuyalinda.

Ameyasema hayo alipokuwa Mgeni Rasmi kweye hadhara ya maadhimisho ya Jumuiya ya Ismaili iliyofanyika Jijini Dar es salaam katika Shule ya Msingi Muhimbili na Umoja wa Mataifa. Mhe. Jafo amesema kuwa kwa Jamii ya Ismaili kufanya sherehe hii kwa kuangazia upande wa mazingira imemfurahisha sana akiwa kama Waziri upande wa mazingira ameona ni jambo jema la kuhamasisha na kusisitiza jamii kusimamia na kulinda mazingira.

“Tumeona mmefanya kwa vitendo Zaidi katika suala la utunzaji wa mazingira na tumeshiriki kwa pamoja katika upandaji miti ambalo ni jambo zuri na inapendeza, itakuwa mfano katika jiji letu la Dar es Salaam na kwa Tanzania Nzima” Amesema Mhe. Jafo

Ameendelea kusema kuwa suala la upandaji miti na kuweka elimu ya mazingira kwa Watoto na uzalendo ni vitu vilimvyomfurahisha sana. Mhe. Jafo amesema kuwa kama Jumuiya mbalimbali za dini zitaiga mfano mzuri unaofanywa na Jumuiya hii ya Ismaili basi Tanzania yetu itakuwa salama kwa upande wa Mazingira.

“Tuendelee kupanda miti na tupunguze matumizi ya mkaa na kuni kwani hali ya kimazingira kwa sasa inatisha sisi Watanzania kwa umoja wetu tuungane kwa pamoja kuepusha athari ya mabadiliko ya Tabianchi. Taifa limeingia katika uchumi wa Kati ili tuweze kwenda mbele Zaidi basi tunahaja ya kulinda na kuhifadhi mazingira yetu.” Amesema Mhe. Jafo

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Ng’wilabuzu Ludigija amesema kuwa Jumuiya hii imeonyesha mfano kwa jumuiya zingine kwani wanashiriki katika masuala mbalimbali ya kijamii ikiwemo usafi na utunzaji wa mazingira pia katika maafa mbalimbali Jumuiya hiyo imekuwa mstari wa mbele.

Naye Mwakilishi wa Taasisi ya Aga Khan Nchini Tanzania Amin Kurji ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kujenga Mazingira wezeshi kwa wawekezaji binafsi katika maendeleo ya jamii ya Tanzania, na jinsi hali hiyo ilivyo muhimu kwa kazi za kuleta mendeleo. Urafiki kati ya Ismaili Imamat na Taasisi zake na Serikali ya Tanzania ni wa muda mrefu na wa manufaa.