KIKOSI KAZI CHA KURATIBU UTEKELEZAJI WA MUONGOZO WA USAFISHAJI MITO MKOA WA DAR ES SALAAM WAKUTANA NA WADAU WA KUCHIMBA MCHANGA KWENYE MITO


Kikosi Kazi cha Kuratibu Utekelezaji wa Muongozo wa Usafishaji Mito na Mabonde Mkoa wa Dar as Salaam wafanya mkutano na wadau wanaojishughulisha na uchimbaji mchanga kwenye mito kutoa ufafanuzi wa muongozo uliotolewa katika usafishaji mito, mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo umefanyika kwa lengo la kuwaelimisha wadau wote wanaojishughulisha na usafishaji mito wakiwemo wakandarasi wakubwa na wale wadogo wanaochimba mchanga kutumia machepe kwa kuwaeleza namna muongozo huo utakavyo waruhusu kufanya kazi kwenye mito kwa kuzingatia sheria ya Mazingira.

Meneja wa Kanda ya Mashariki Kaskazini Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Bw. Arnold Mapinduzi ambaye ni mjumbe wa Kikosi Kazi cha Kuratibu Utekelezaji wa Muongozo wa Usafishaji Mito, amesema kuwa hali ya mazingira iliyopo kwa sasa kwenye mito yetu ni mbaya sana, utoaji wa mchanga ulikuwa unafanyika kiholela hivyo kwa sasa kuna muongozo umepitishwa ambao kila mtu anatakiwa kuufuata na kuzingatia masharti yake ili kuepusha athari katika mazingira yetu

Ameendelea kusema kuwa jukumu la kulinda mazingira ni jukumu letu sote, hivyo kila mmoja wetu akawe mlinzi wa mwenzie ili kuepusha athari za kimazingira katika jamii yetu.

"Lengo la kuundwa kamati hii ni kuhakikisha usafishaji mchanga kwenye mito unatekelezwa kwa kuzingatia sheria ili kuhakikisha tunaishi kwenye mazingira safi na salama na hatusababishi madhara kwa jamii yetu" amesema Bw. Mapinduzi

Kwa upande wake Mjumbe mwingine wa Kikosi kazi hiko Bw. Mshuda Wilson ni kutoka Wizara ya Maji-Bonde la Wami Ruvu, amesema kuwa wale wote wanaojishughulisha na uchimbaji mchanga kwenye mito wanatakiwa kufanya maombi ya kibali upya kwa kuzingatia muongozo uliotolewa.

" Hitaji la kusafisha mito ni kubwa ili kuepusha madhara ya kimazingira kama mafuriko, hii ni kutokana na kujaa kwa uchafu na mchanga katika mito yetu hivyo kutokana na hayo ni vizuri kusafisha mito kwa kuzingatia sheria na miongozo ili kuepusha athari katika jamii" amesema Bw. Mshuda

Bw. Mapinduzi amemalizia kwa kusema kamati imepokea maombi 45 mpaka sasa, ambayo 23 ni ya wanaochimba kwa machepe na 22 ni ya wakandarasi. Katika maombi hayo, kati ya maombi 23 kutoka kwa wanaochimba kwa machepe ni 8 tu ndio waliokidhi vigezo ambao watapewa kibali na kati ya wakandarasi 22 ni 12 tu ndio wamekubaliwa kupewa kibali, 12 hawakukidhi vigezo na watatakiwa kufanya marekebisho kidogo ila 2 wamekataliwa kabisa.

"Naomba kuwakumbusha kuwa pale unapopewa kibali hakikisha unazingatia sheria na muongozo uliotolewa endapo utakiuka masharti faini ya kiwango cha chini kisichopungua 3,000,000 na adhabu nyingine zitafata, lengo ni kukufanya uzingatie sheria na si vinginevyo" Bw. Mapinduzi

Kikosi Kazi cha Kuratibu Utekelezaji wa Muongozo wa Usafishaji Mito, kiliundwa baada ya kutolewa maagizo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira baada ya kukutana na Wadau wanaojishughulisha na biashara ya usafishaji mito na kusikiliza changamoto zao.