DKT. GWAMAKA AFURAHISHWA NA VIWANDA NCHINI KUZALISHA VIFUNGASHIO VINAVYOKIDHI TAKWA LA KISHERIA


Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Muhandisi Samuel Gwamaka, amesema kuwa amefurahishwa sana na wazalishaji wa viwanda kuzalisha vifungashio vinavyokidhi takwa la kisheria na pia kuwepo kwaviwanda vinavyoweza kurejeleza vifungashio hivyo na kuepusha athari mbalimbali za kimazingira.

Ameyasema hayo katika Mkutano wa waandishi wa habari ulioandaliwa na Shirikisho la wenye viwanda Nchini (CTI) uliofanyika hivi leo katika ukumbi wa Hotel ya Four Point by Sheraton jijini Dar es Salaam

" Nimefurahishwa sana na viwanda Nchini kuweza kuzalisha vifungashio vinavyokidhi viwango na kuweza kuanzisha viwanda vitakavyo rejeleza vifungashio hivyo baada ya kutumika. Katazo la vifungashio vya plastiki visivyokidhi viwango linalenga katika kuzuia uchafu wa mazingira katika Nchi yetu

Aidha, ameendelea kusema kuwa kwa pamoja kwa kushirikiana na wazalishaji, wasambazaji na watumiaji watahakikisha wanazingatia takwa la sheria kwa kutumia vifungashio vitakavyo kidhi vigezo na kuepusha athari katika mazingira .

Pia ningeomba wazalishaji waendelee kutoa elimu kwa wasambazaji na watumiaji ili kuweza kufikia malengo ya serikali." Amesema Dkt.Gwamaka.

Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), limeandaa mkutano huo kwa ajili ya kutoa elimu kwa umma juu ya vifungashiovya plastiki vinavyokidhi viwango, Ikiwa leo ni kilele cha matumizi ya vifungashio vya plastiki visivyokidhi vigezo na ambavyo vinaweza kurejelezwa kutokana na ubora wa uzalishaji wa vifungashio hivyo.

Mwakilishi wa Mwenyekiti wa shirikishola Viwanda Tanzania Bw. Sufiani Hussein ameeleza kuwa lengo la mkutano ni kuonesha namna gani viwanda vya uzalishaji wa mifuko ya plastiki wametekeleza agizo lililotolewa na serikali la kuhakikisha viwanda vinazalisha vifungashio vinavyokidhi viwango na vinavyoweza kurejelezwa

" kutokana na agizo la serikali kwanza nichukue fursa hii kuwashukuru NEMC kwa Kushirikiana na TBS kwa kutupa muda wa kujiandaa ili kuwezesha viwanda kupata ufumbuzi wa kuwa na viwanda vya kurejeleza vifungashio vitakavyo zalishwa na natoa shukrani ya dhati kwao kutupa elimu kwa kipindi chote mpaka leo kufikia mwisho wa matumizi ya vifungashio visivyo na vigezo"amesema Sufiani yetu.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Kemilembe Mutasa, amesema kuwa Ofisi yake imefanya tafiti katika baadhi ya masoko na kugundua baadhi ya vifungashio vinavyokidhi viwango vipo masokoni japo sio vya kutosha, hivyo amewaomba wenye viwanda waendelee kuzalisha na kutoa elimu kwa wananchi ili kutekeleza takwa hilo la kisheria.

Mkutano huo umeudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. MuhandisiSamuel Gwamaka, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Kemilembe Mutasa, watumishi wa NEMC, Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Wanahabari, wazalishaji wa vifungashio vya plastiki na wasambazaji.